We use necessary cookies that allow our site to work. We also set optional cookies that help us improve our website. For more information about the types of cookies we use, visit our Cookies policy.

Cookie settings

Tangazo la Kigali kuhusu Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuuzwa

kigali declaration

Tangazo la Kigali kuhusu Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuuzwa

Maendeleo ya ajabu yamefanywa dhidi ya magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa (NTDs) – kikundi cha magonjwa 20 yanayodhoofisha, kuharibu umbo na kuweza kuua. Nchi arubaini na tatu zimeondoa angalau NTD moja, watu milioni 600 hawahitaji tena matibabu ya NTDs, na visa vya baadhi ya magonjwa haya ambayo yamesumbua wanadamu kwa karne nyingi, kama vile malale na ugonjwa wa minyoo ya Guinea, yako katika kiwango cha chini kabisa. Hili linathibitisha kwamba kumaliza NTDs[1] kunawezekana.

Mambo mengi yanategemeza mafanikio haya, lakini mawili ni muhimu kihususa ikiwa mafanikio yataendelea.

Ya kwanza ni uwajibikaji wa nchi na kanda. Iwapo nchi hazingekubali malengo ya kimataifa, kuyageuza kuwa mikakati ya kitaifa na kisha kuyatimiza, maendeleo hayangewezekana. Ni muhimu kwamba nchi ziendelee kuongoza na kuwajibika kumaliza NTDs ikiwa tutaendelea kuona matokeo halisi katika kiwango.

Pili, harakati ya kumaliza NTDs imefafanuliwa na mashirika na ushirikiano baina ya washikadau wa nyanja mbalimbali. Hii inajumuisha shirika kubwa zaidi ulimwenguni la umma-binafsi, ambapo washirika wa viwanda, nchi zinazofadhili, ufadhili wa kibinafsi, taasisi za utafiti na mashirika ya asasi za kiraia yalikuja pamoja ili kuunga mkono Tangazo la London kuhusu NTDs[2] katika kuunga mkono kutimizwa kwa mwongozo wa NTD wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) ya kwanza. Ushirika huu lazima upanuliwe na kuendelezwa, na nchi na jamii zilizoathiriwa zikiwa katikati. Ni kupitia tu hatua iliyoratibiwa na ushirikiano, na kila mshiriki akitimiza sehemu yake,ndivyo tunaweza kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya UN (SDGs) na kutimiza tamaa za mwongozo wa NTD wa WHO ya 2030, ambayo inatia ndani kuondolewa ulimwenguni kwa magonjwa mawili (ugonjwa wa minyoo ya Guinea na minyoo ya yaw) na kuondolewa kwa angalau NTD moja katika nchi 100.

Jitihada za kukabiliana na NTDs ni hadithi ya mafanikio ya afya ulimwenguni, lakini bado kuna kazi nyingi zaidi inayohitaji kufanywa kabla ya ulimwengu kuwa huru kutokana na NTDs[3] – magonjwa haya kwa sasa yangali yanaathiri watu bilioni 1.7. COVID-19 pia imeathiri huduma muhimu za afya ulimwenguni pote, huku programu za NTD kihususa zikiwa zimeathiriwa vibaya. COVID-19 pia imeonyesha umuhimu mkubwa wa kuwekeza katika mifumo thabiti ya afya ya msingi inayoweza kushughulikia magonjwa yaliyoenea, kama vile NTDs, na kuufanya ulimwengu kuwa mstahimilivu zaidi kuelekea majanga.

Hatua ya pamoja inahitajika ili kuepuka COVID-19 na majanga yajayo kurudisha nyuma maendeleo ya miaka mingi na kuhatarisha mamilioni ya watoto kwa magonjwa yanayoweza kuepukika. Tuna fursa kubwa sasa hivi ya kubadili maisha ya wale walioathiriwa na NTDs, ambao mara nyingi wamenaswa katika mizunguko ya umaskini mkubwa kwa kuzuiwa kuenda shuleni au kuweza kufanya kazi. Magonjwa haya yanaweza kuepukika au kutibika, kwa hiyo tuna uwezo wa kumaliza NTDs.

Kwa hivyo, kila mmoja wetu anaahidi kufanya sehemu yake katika kiwango cha ulimwengu, kanda, nchi, jamii na mashirika ili kuhakikisha kwamba NTDs zinatokomezwa, kumalizwa au kudhibitiwa kufikia 2030.

Tangazo la Kigali kuhusu Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuuzwa

Kwa kujenga katika maendeleo ya Tangazo la London kuhusu Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuuzwa (NTDs) na kuweka watu binafsi na jamii katikati ya itikio la NTD, sisi, watiaji sahihi wa tangazo hili, tunakuja pamoja ili kuazimia kumaliza NTDs[4].

Tunatambua kwamba NTDs ni magonjwa ya umaskini na ukosefu wa usawa. Kwa kukabiliana na NTDs tutapunguza umaskini, kushughulikia ukosefu wa usawa, kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza mtaji wa binadamu na kujenga jamii stahimilivu, hivyo kutuleta karibu zaidi na kutimiza maandalizi ya afya kwa wote na SDGs. Tangazo hili ni la na kwa ajili ya watu bilioni 1.7 wanaoendelea kuteseka kutokana na NTDs.

Watiaji sahihi wote wa tangazo hili wanaazimia kuhakikisha kutimizwa kwa lengo la 3 la SDG[5] linalolenga NTDs na [6] kutekelezwa kwa mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030: Kukomesha upuuzaji ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu: mwongozo kwa ajili ya magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa 2021−2030[7]. Kwa pamoja tumeazimia kushikamana na kanuni ya ‘usifanye madhara yoyote’ na tutatekeleza kulingana na maazimio na michango yetu yaliyoelezwa katika tangazo hili kwa:

● Kufanya kazi kuhakikisha watu walioathiriwa – hasa wanawake na wasichana, watu wenye ulemavu, na vikundi vidogo na visivyowakilishwa kikamili – wako katikati ya programu za NTD na michakato ya kufanya maamuzi.

● Kuwa mabingwa na mabalozi wa kukabiliana na NTDs kwa kuongeza utambulisho na umuhimu wa NTDs mashinani, nchini, katika kanda na ulimwenguni na kuhakikisha NTDs zinapewa kipaumbele katika viwango vya juu zaidi.

● Kuendeleza mtazamo wa sekta nyingi na wa fani mbalimbali katika kukabiliana na NTDs, kutia ndani One Health, inayotambua ushirikiano wa afya ya binadamu, wanyama na mazingira na muktadha mpana zaidi wa jamii, tamaduni na uchumi.

● Kuongeza uandalizi wa huduma zinazowezesha ufikiaji sawa wa kuzuia, kuchunguza, kutibu na udhibiti wa magonjwa ya NTDs.

● Kufungua rasilimali za nchi, kutia ndani kuimarisha miundombinu ya afya ya umma ili kutekeleza programu zenye matokeo za NTD, zinazokamilishwa na rasilimali kutoka nje.

● Kutambua fursa za ufadhili endelevu na kuwa wasimamizi wa rasilimali zilizopo ili kuongeza matokeo na thamani ya pesa.

● Kufanya kazi kwa njia iliyoratibiwa na kuunganishwa iliyokita katika matibabu ya msingi na iliyopachikwa ndani ya mifumo stahimilivu ya kitaifa inayohudumia jamii zilizoathiriwa.

● Kuwekeza katika utafiti na uvumbuzi wa dawa na uchunguzi mpya kwa ajili ya maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030 na, inapofaa, kusaidia kuhamishwa kwa teknolojia na ufadhili ili kuhakikisha kuna usambazaji endelevu wa bidhaa kwa ajili ya NTDs.

● Kuboresha ukusanyaji na utumiaji wa data ili kulenga programu, kuongeza manufaa yake na kuharakisha maendeleo.

● Kufuatilia na kuripoti kwa uwazi maendeleo yaliyofanywa katika maazimio na michango iliyoelezwa katika tangazo hili, kumfanya mmoja na mwenzake wawajibike huku tukiunga mkono uwajibikaji wa kitaifa kwa programu za NTD za nchi.

Kwa kufanya kazi pamoja, kutumia mitazamo ya kuweka watu katikati na kufanya kazi katika sekta mbalimbali, tunaweza kufikia na kuendeleza lengo la SDG kuhusu NTDs na malengo katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030. Tunaweza kukomesha magonjwa mawili, kuondoa angalau ugonjwa moja katika nchi 100, na kupunguza idadi ya watu wanaohitaji uingiliaji kati wa NTDs kwa 90%. Maazimio haya yatasaidia kupunguza kuteseka, kupunguza visababishi vya umaskini vinavyohusiana na afya, kupunguza ulemavu na unyanyapaa, na kuboresha halinjema ya kiakili na ujumuishaji katika jamii.

Maazimio na Michango ya Wadau

Kufikia malengo yaliyotajwa katika tangazo hili kunategemea makundi yote ya wadau kufanya kazi pamoja ili kutimiza majukumu yao. Kila mdau hutoa mchango wa kipekee na muhimu. Kwa pamoja haya hutokeza maendeleo kufanyika.

Kama serikali za kitaifa

Tunaazimia kudhihirisha uongozi wa kisiasa na umiliki wa nchi kwa:

● Kupachika programu za uingiliaji kati za NTD katika mifumo yetu ya afya ya kitaifa.

● Kuhakikisha programu za kuzuia, kuchunguza na kutibu NTDs zinapewa kipaumbele, zinapata rasilimali kikamilifu na kuunganishwa kikamilifu ndani ya mipango ya mikakati ya kitaifa ya wizara za afya na zinazohusiana nayo (kama vile kilimo, afya ya mifugo, maji na usafi, masuala ya jinsia na familia, na mazingira), kufuatilia mtazamo wa One Health.

● Kutoa mgawo wa kutosha wa fedha na maazimio kuelekea uingiliaji kati wa NTD.

● Kutumia vizuri michango ya dawa za NTD kutoka kwa washirika wa viwandani kwa kuhakikisha kwamba rasilimali zinazohitajika ili kufikisha dawa hizi zinapatikana.

● Kuboresha ufuatiliaji wa ugonjwa, kutengeneza ramani ya magonjwa, na jinsi data inavyokusanywa na kutumika – kutia ndani kupitia kuboresha matumizi ya kidijitali – ili kulenga na kufikisha dawa zilizotolewa kwa njia bora zaidi.

● Kuondoa vizuizi vya ufikiaji kama vile kodi za kibali za dawa za NTD zilizotolewa ili kuhakikisha kwamba hizi zinasambazwa kwa jamii zisizojiweza kwa wakati.

● Kutengeneza sera za kitaifa za afya ya umma za kuzuia na kutibu NTD.

● Kuhakikisha mifumo ya usimamizi wa habari za afya ipo ili kusimamia data za programu ya NTD na kuandaa ripoti za kifedha na za programu kuhusu viashiria muhimu vya utendaji wa kitaifa wa programu za NTD.

● Kuripoti kuhusu maendeleo ya kitaifa ya NTD ikiwa sehemu ya kufuatilia na utaratibu wa kupitia wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030[8].

● Kubadili kutoka kwa kupokea michango mikubwa ya dawa hadi kuandaa uchunguzi na dawa muhimu na nafuu katika mifumo yetu ya afya – kuanzia wale walio na uhitaji zaidi na kutumia rasilimali za nchi kwa ushirikiano na sekta ya kibinafsi. (Uendelezaji utategemea kuendelea kupokea michango hii kwa muda mfupi na kubadili kwa kuongeza kufikia ununuzi na ufadhili wa nchi wa uchunguzi na dawa katika muda wa kati kuelekea mrefu.)

Kama wabunge

Tunaazimia:

● Kutumia wenzo za kisiasa tulizo nazo ili kutokeza ufahamu kuhusu gharama ya kibinadamu ya NTDs – magonjwa yanayoweza kuzuiwa na kutibiwa.

● Kupendekeza na kupitisha sheria na bajeti zinazoonyesha mapendezi ya kisiasa, uongozi na kuwajibika kuelekea kumaliza NTDs[9].

● Kuongeza ufahamu wa faida za usalama wa kiafya wa ulimwengu za kuunga mkono programu za NTD katika kiwango cha kitaifa.

Kama mameya na viongozi wa serikali ya mtaa katika nchi zilizoathiriwa

Tunaazimia:

● Kutumia nafasi yetu kama madalali kati ya mamlaka za kitaifa na jamii za eneo ili kuharakisha maendeleo yaliyounganishwa ya vijijini na mijini na kutengeneza mazingira mazuri na yenye mafanikio.

● Kushiriki na kuwezesha jamii na viongozi wake kutambua changamoto za eneo lao za afya ya umma kama vile NTDs na sababu za hatari zinazoendelea katika eneo.

● Kutafuta suluhisho za kinyumbani zinazotegemea ushahidi za NTDs na changamoto zinazohusiana za afya ya umma na kuwajibika kuelekea kutekelezwa kwazo.

● Kuratibu huduma katika sekta mbalimbali ili kuboresha mazingira yaliyojengwa – ikijumuisha makazi, utengenezaji na udumishaji wa miundombinu, maji na usafi, na utupaji taka ulio salama kimazingira – ili kupunguza usambaaji wa NTDs na magonjwa mengine ya kuambukiza.

● Kufanya kazi na mashirika ya asasi za kiraia (wanaoandaa daraja muhimu kati ya serikali ya mtaa na jamii zilizo ngumu kufikiwa), serikali ya kitaifa, sekta ya kibinafsi na wadau wengine muhimu katika kukomesha NTDs[10].

● Kuhakikisha wanawake, vijana, watu wenye ulemavu, na vikundi vidogo na visivyowakilishwa kikamili wanajumuishwa katika michakato ya kutengeneza sera na kufanya maamuzi.

Kama mabaraza ya bara na kanda

Tunaazimia:

● Kuandaa uongozi wa kisiasa kwa ajili ya utambulisho wa NTDs kama vipaumbele katika afya na maendeleo katika kanda zetu.

● Kuunga mkono hatua iliyoratibiwa ya sekta nyingi dhidi ya NTDs katika nchi ambazo ni wanachama.

● Kupitia maendeleo katika kukomesha NTDs[11] na kuchukua hatua za lazima za kurekebisha mwendo.

● Kusherehekea nchi zinapotimiza hatua muhimu.

● Kuonyesha na kuongoza mazoea bora zaidi kuelekea kukomesha NTDs.

● Kuandaa jukwaa, kama vile Kadi ya Alama ya ALMA, ili kuunga mkono kuwajibika kikanda kuelekea kufikia malengo ya NTD katika nchi ambazo ni wanachama.

● Kupanga, na inapowezekana kuoanisha, kuidhinishwa kwa na utengenezaji wa miongozo ya vifaa vya kuzuia na kutibu NTDs, kupunguza wakati unaohitajika kwa uchunguzi mpya, dawa na chanjo kupitishwa.

● Kuandaa jukwaa la mipango ya kimkakati inayopita mipaka na kusawazisha uingiliaji kati ili kudhibiti NTDs.

● Kutetea udhibiti na uondoaji wa NTDs kati ya nchi ambazo ni wananchi na wadau wengine muhimu.

● Kuandaa majukwaa ya kuita mikutano na vikao ambayo itakuza utetezi na ushirikiano kwa ajili ya kudhibiti na kuondoa NTDs.

Kama Umoja wa Mataifa

Tunaazimia kuandaa uongozi wa ulimwengu na utetezi wa ufikiaji sawa wa afya na maendeleo kwa ajili ya watu na jamii zilizoathiriwa na NTDs, kupatana na kanuni za SDGs na maandalizi ya afya kwa wote, kutoacha yeyote nyuma.

Kama WHO

Tunaazimia, kupitia mtandao wetu wa ofisi za WHO:

● Kuandaa uongozi wa afya ulimwenguni – pamoja na utegemezo na mwongozo wa kiufundi na wa programu – kwa nchi zinapotekeleza programu zao za kitaifa za NTD kama ilivyopendekezwa katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

● Kufuatilia na kuripoti maendeleo kuelekea malengo ya mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

● Kuandaa miongozo ya sera kwa wakati ili kuunga mkono uboreshaji wa haraka wa uungaji mkono wenye mafanikio dhidi ya NTDs.

● Kutengeneza itifaki bora za ufuatiliaji na utathmini na miongozo kwa programu na nchi.

● Kuthibitisha, kuhalalisha au kuhakikisha kuondolewa au kumalizwa kwa ugonjwa.

● Kutumia data kutoka kwa mifumo ya habari za afya ya kitaifa kama chanzo kikuu cha habari kwa ajili ya kufanya maamuzi.

● Kuunga mkono nchi katika kuanzisha na kuimarisha mifumo yao ya habari za afya ya kitaifa.

Kama sekta ya kibinafsi na kampuni za dawa

Tunaendelea kuazimia:

● Kuunga mkono programu za NTDs za kitaifa na kimataifa za ufikiaji wa dawa – kupatana na mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030 – kupitia uwajibikaji wetu wa michango ya dawa na uchunguzi unaotegemeka, salama na thabiti, unaotegemezwa na ufadhili kutoka kwa wafadhili na serikali ili kudhibiti, kuondoa na/au kumaliza NTDs.

● Kuunga mkono Utafiti na Maendeleo ya matibabu mapya, na ufikishaji wake kwa watu na programu kwa ajili ya uboreshaji salama na wenye mafanikio, kama inavyohitajika ili kufikia malengo ya mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030 na zaidi.

● Pamoja na washirika wa kitaifa na kimataifa, kutengeneza kwa pamoja suluhisho imara ya mifumo endelevu ya afya ya kieneo inayoboresha mipango yenye mafanikio ya kubadilisha ya nchi binafsi inayodhibitiwa na wakati inayotamani mwishowe kujisimamia kifedha bila usaidizi na matokeo ya muda mrefu yenye faida.

Kama wafadhili

Sisi, kama wafadhili wa sekta za umma na kibinafsi, tunaazimia kupeana rasilimali zetu za kiufundi na kifedha ili kuunga mkono nchi zifikie malengo ya mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030 kwa:

● Kushirikiana na kufanya kazi pamoja na nchi zilizoathiriwa na ugonjwa ili kuunga mkono mipango yao na usimamizi wa rasilimali ili zifikie malengo ya magonjwa hususa huku wakijenga mifumo stahimilivu ya afya.

● Kushirikisha wafadhili wengine ili waunge mkono NTDs na kuimarisha usimamizi wa ufadhili chini ya uongozi wa nchi zilizoathiriwa na magonjwa.

● Kuwezesha ufadhili endelevu kupitia kufanya kazi pamoja na michakato ya ufadhili nchini na kuhakikisha rasilimali za wafadhili wa NTD zinatosheleza badala ya kudhoofisha au kuwa badala ya rasilimali za nchi.

● Kufanya kazi na serikali za nchi, taaluma, WHO na viwanda ili kufadhili utafiti wa matibabu na uchunguzi mpya ili kuharakisha maendeleo dhidi ya NTDs kupatana na vipaumbele vya nchi zilizoathiriwa na magonjwa.

Kama mashirika ya kimataifa

Tunaazimia:

● Kuwekeza katika kuimarisha mifumo ya afya kwa kuendelea kuunga mkono utoaji huduma uliounganishwa na kuendelea kufadhili uingiliaji kati wa programu muhimu zinazounga mkono uingiliaji kati wa programu za NTD.

● Kutetea mipango imara ya kimkakati ya kitaifa inayoongozwa na matokeo ya NTDs, kuunga mkono nchi katika utengenezaji wa mipango yao ya kimkakati ya kitaifa kuhusu kuondoa NTD, na kuunga mkono nchi katika kutekeleza programu zao za NTD.

● Kuhamasisha rasilimali katika kuunga mkono programu za kitaifa za NTD, uchunguzaji na utokezaji wa dawa.

● Kufanya NTDs kuwa nguzo ya Mpango wa Hatua ya Ulimwenguni ya One Health[12] chini ya Muungano Mkuu wa Pande Tatu (WHO, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, Shirika la Dunia la Afya ya Wanyama, na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa) ndani ya mpango mpana zaidi wa kuongeza uwezo, uratibu wa sekta nyingi na ugawaji wa rasilimali.

Kama mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na kijamii

Tunaazimia:

● Kuratibu michango yetu kama washiriki watekelezaji pamoja na nchi zenye magonjwa ili kufikia malengo ya mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030, kutia ndani kutetea kuongezwa na kuendelelezwa kwa rasilimali za nchi kwa ajili ya programu za NTD, ili kuimarisha uwezo wao wa kifedha.

● Kuwezesha kushiriki kulikoboreka kwa jamii zilizoathiriwa na NTDs katika viwango vyote vya uundaji wa programu ya NTD, utekelezaji, sera, utafiti, ufuatiliaji na utathmini.

● Kulinda jamii zilizoathiriwa na NTDs kupitia mtazamo wa ‘usifanye madhara yoyote,’ huku tukihusisha sehemu zote za jamii hizi katika vita dhidi ya NTDs na kujenga mitandao ya kieneneo ya mabingwa wa NTD ili kuunga mkono utetezi, malengo ya kijamii na uhamasishaji wa rasilimali.

● Kuanzisha mazoea ya ushahidi unaotegemea ujuzi – kwa msingi wa data imara – kwa ajili ya kutekelezwa kwa uingiliaji kati endelevu unaounga mkono mifumo stahimilivu ya afya na programu iliyojumuishwa kwa kiwango na kwa matokeo.

● Kupitisha mtazamo unaojumuisha katika kutambua, kutekeleza, kufuatilia na kutathmini miradi na programu za NTD, kufikiria vipengee vya kijinsia na mahitaji hususa ya sehemu mbalimbali za idadi ya watu (k.m. watu wenye uwezo uliopungua wa kutembea, wanawake, wanaume, vijana na wazee).

Kama taasisi za masomo na utafiti

Kwa kupatanisha sekta zetu na mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030 na kufanya kazi pamoja na nchi zilizoathiriwa, tunaazimia:

● Kutekeleza ajenda ya utafiti ulioratibiwa na unaoongozwa na nchi unaokazia zaidi kuimarisha uwezo wa kitafiti, uvumbuzi, ufikiaji na usawa.

● Kukuza utafiti wa fani mbalimbali (unaotia ndani matibabu na sayansi ya kijamii) ili kujenga uelewaji bora zaidi kati ya fani mbalimbali wa jinsi NTDs hufanya kazi, ikijumuisha jinsi programu za NTD zinavyoweza kuingizwa kwa mafanikio katika mifumo ya afya ya kieneo na kitaifa, na jinsi ujuzi huu unavyoweza kugeuzwa kuwa sera na mazoea.

● Kushirikiana na jamii katika kutokeza uingiliaji kati unaoweza kushughulikia kwa mafanikio mahitaji tata ya watu walioathiriwa na NTDs katika muktadha wao wa kitaifa na kieneo na, mwishowe, kufanya hatua dhidi ya NTDs kuwa mwelekeo wa kuimarisha mifumo ya afya.

● Kuendeleza mitaala kina ya elimu kuhusu kuzuia, kutibu na kudhibiti NTDs katika hatua zote za maendeleo ya elimu ulimwenguni, kwa kuzingatia kuongeza uwezo na ubora wa wafanyikazi wa kiafya na utafiti na katika kutengeneza mazingira yanayowezesha kwa ajili ya ushirikiano wa kimataifa ili kuvutia na kuunganisha wataalamu wengi muhimu wanaofanya kazi katika nchi zenye magonjwa.

● Kutetea ongezeko katika gharama ya Utafiti na Maendeleo ya afya (umma na binafsi, kama uwiano wa GDP) na katika gharama za afya ya kitaifa (katika uvumbuzi wa kitafiti na kuimarisha uwezo), kulingana na SDGs.

● Kuunga mkono ukuzi wa taratibu imara za ufuatiliaji na utathmini katika sekta mbalimbali zinazoweza kupima matokeo ya kudhibiti, kuondoa na kumaliza NTDs.

Kama vijana

Tunaazimia:

● Kutumia sauti zetu ili kushiriki, kuwezesha na kuunga mkono jamii za vijana na viongozi vijana – ikijumuisha vijana walio na ulemavu – kuelekea kutekeleza na kufikia mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030, na hivyo kuhakikisha kwamba vijana hawaachwi nyuma katika vita dhidi ya NTDs.

● Kuleta ubunifu wetu, nguvu zetu, hisi yetu ya uvumbuzi, stadi zetu za teknolojia mpya, fikira zetu, na talanta zetu katika vita dhidi ya magonjwa haya.

● Kushiriki na kuunga mkono mabaraza ya kufanya maamuzi ya kimataifa, kikanda na ya nchini katika kutekeleza utetezi na kutekeleza mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

● Kukuza na kukubali mazoea mazuri yanayozuia NTDs na kuunga mkono afya ya kiakili na halinjema.

[1] Kwa kusema ‘maliza NTDs’ tunamaanisha NTDs zinadhibitiwa, kuondolewa au kutokomezwa, kama ilivyoonyeshwa katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

2 Tangazo la London kuhusu NTDs: https://unitingtocombatntds.org/resource-hub/who-resources/london-declaration-neglected-tropical-diseases/

3 Mwongozo wa NTD wa WHO 2012–2020: https://www.who.int/neglected_diseases/NTD_RoadMap_2012_Fullversion.pdf

4 Kwa kusema ‘huru kutokana na NTDs’ tunamaanisha NTDs zinadhibitiwa, kuondolewa au kutokomezwa, kama ilivyoonyeshwa katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

5 Kwa kusema ‘maliza NTDs’ tunamaanisha NTDs zinadhibitiwa, kuondolewa au kutokomezwa, kama ilivyoonyeshwa katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

6 https://sdgs.un.org/goals

[7]Mwongozo wa NTD wa WHO na hati zinazoambatana: https://www.who.int/publications/i/item/9789240010352

[8] https://sdgs.un.org/2030agenda

[9] Kwa kusema ‘maliza NTDs’ tunamaanisha NTDs zinadhibitiwa, kuondolewa au kutokomezwa, kama ilivyoonyeshwa katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

[10] Kwa kusema ‘maliza NTDs’ tunamaanisha NTDs zinadhibitiwa, kuondolewa au kutokomezwa, kama ilivyoonyeshwa katika mwongozo wa NTD wa WHO wa 2030.

[11] Ibid.

[12] https://www.who.int/groups/one-health-high-level-expert-panel